Uhusika katika Fasihi Bulibuli ya Kiswahili: Mfano Kutoka Utenzi wa Mikidadi na Mayasa
الملخص
Makala hii inatathmini uhusika wa wahusika katika tenzi za Kiswahii kwa kuegemea utenzi mmoja bulibuli: Utenzi wa Mikidadi na Mayasa. Utenzi huu ulitungwa na Saidi Abdallah Masudi el Buhry aliyekuwa mkazi wa Pemba. Ingawa Masudi aliishi Pemba kwa muda, alihamishwa kwenda Mtang’ata, kilomita kumi kusini mwa Tanga alipohudumu kama gavana wa utawala wa Kimazrui. Bwana Masud alikuwa mshairi mtajika kwa tungo zake nyingi. Utenzi huu ni mmojawapo wa kazi zake zilizotia fora katika janibu ya Waswahili wakati huo. Allen (1971) anasema kuwa utenzi wa Mikidadi na Mayasa unahusu mashujaa wa wakati wa mtume Mohammed (SAW) na baada ya kufariki kwake. Kipengele cha wahusika ni muhimu katika kutunga kazi yoyote ya kifasihi. Kinashirikishwa na vipengele vingine vya kifani ili kuwezesha mtunzi kutoa maudhui au ujumbe wake. Watunzi wa kazi ya kifasihi huwajenga wahusika kisanaa ili waweze kuwakilisha vipengele vingi katika maisha ya jamii wanayotungia. Watunzi pia hutumia mbinu mbalimbali kuwasawri wahusika kutegemea tajriba yao ya kisanii pamoja na utanzu unaoshughulikiwa. Makala hii inafafanua baadhi ya mbinu zilizotumiwa na mtunzi kuwajenga wahusika wa aina mbalimbali waliojitokeza katika Utenzi wa Mikidadi na Mayasa. Pia inabainisha kuwa ushairi, hasa tenzi huwa na wahusika waliojengwa kikamilifu kwa kutumia mbinu mbalimbali za kimtindo na za lugha. Huu ni utafiti wa maktabani. Uliongozwa na nadharia ya Umitindo hasa mawazo ya Leech (1969). Alisisitiza umuhimu wa lugha kama chombo tekelezi kinachosaidia mtunzi wa kazi ya fasihi kuwasilisha ujumbe wake. Uchanganuzi wa matini za kifasihi kwa kutumia Umitindo unaweza kutekelezwa kwa kuchunguza jinsi mwandishi amefinyanga lugha kisanii ili kuwasilisha ujumbe, kuchunguza msuko na sifa za kimuundo za kazi, mbinu za usimulizi na mikabala ya kimtazamo anayochukua mwandishi Aidha, Umitindo unahusisha uchunguzi wa uteuzi wa wahusika, mandhari na lugha yao, hulka na sifa zao zinazowezesha mtunzi kuwatumia kuakisi masuala fulani katika jamii anayotungia. Nadharia hii ilikuwa muhimu katika utafiti huu uliolenga kutathmini uhusika au mikakati iliyotumiwa na mtunzi kuwasawiri wahusika. Wahusika kama nyenzo kuu huteuliwa, kukuzwa na kuendelezwa na msanii kimaksudi ili waweze kukuza dhamira na maudhui. Nadharia hii ilimwezesha mtafiti kuchunguza mbinu za lugha na za kimtindo zilizotumiwa kuwasawiri wahusika. Makala hii imegawika katika sehemu tatu; sehemu ya kwanza ni utangulizi unaotoa muhtasari kuhusu Utenzi wa Mikidadi na Mayasa. Sehemu ya pili inaangazia dhana ya wahusika katika fasihi na sehemu ya tatu inafafanua uhusika kwa jumla, sehemu ya nne inabainisha mbinu zilizotumiwa kuwasawiri wahusika katika Utenzi wa Mikidadi na Mayasa
التنزيلات
المراجع
Culler. J. (1975). Structuralist Poetics: Structuralism, Linguistics and the Study of Literature. London: Routledge & Kegan Paul.
Forster, E.M. (1927). Aspects of the Novel. London: Penguin Books
Kingei, K. & Kemoli, A. (2001). Taaluma ya Ushairi. Acacia Stantex Publisers.
Leech, G. N. (1969). A Linguistic Guide to English Poetry. Longman Group Ltd.
M’Ngaruthi, T.K. (2007). Usawiri wa Wahusika katika Dafina ya Umalenga na Jicho la Ndani. Tasnifu ya Uzamili (haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Kenyatta
M’Ngaruthi, T.K (2019). Umbuji wa wahusika Katika Ushairi wa Kiswahili: Mifano kutoka kwa Diwani ya Jicho la ndani katika East African Scholars Journal of Education, Humanities and Literature (vol.2 Toleo la 6) uk.296-300
M’Ngaruthi. T.K. (2015). Usawiri wa Mwanasiasa wa Afrika katika Ushairi wa Kiswahili. Tasnifu ya Uzamifu (haijachapishwa) Chuo Kikuu cha Chuka.
Msokile, M. (1993). Misingi ya Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: East Africa Educational Publisher
Mulokozi, M. (1996). Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam: Tasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili
Njogu, K. & Chimerah, R. (1999). Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Wamitila, K. W. (2002). Uhakiki wa Fasihi: Msingi na Vipengele vyake. Nairobi: Phoenix Publishers Ltd.
Wamitila, K. W. (2003). Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. Nairobi: Focus Publishers Ltd.
Wamitila, K. W. (2008). Kanzi ya Fasihi: Misingi ya Uchanganuzi wa Fasihi Nairobi: Vide-Muwa Publishers Ltd.
الحقوق الفكرية (c) 2024 Rosemary Njeri Burundi, Allan Mugambi, PhD, Timothy Kinoti M’Ngaruthi, PhD

هذا العمل مرخص حسب الرخصة Creative Commons Attribution 4.0 International License.